Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ametembelea Wilaya ya Kongwa na kuongea na wananchi wa Kongwa katika viwanja vya Ofisi ya Mbunge. Rais Magufuli ameongeza na wananchi baada ya kutoka kutembelea kaburi alikozikwa baba yake Mhe Joab Ndugai ambaye ni Spika wa Bunge la Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa.
Katika ziara hii, Rais Magufuli ametoa maagizo mbalimbali alipokuwa akiongea na wananchi Wilayani Konbwa.
Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli ameagiza Wizara Katiba na Sheria pamoja na vyombo vingine vya ulinzi vinavyohusika na Mahakama wapitie magereza yote nchini huko wakae wazungumze na watuhumiwa waliopo mahabusu ili kubaini mahabusu wote wanaoshikiliwa kimakosa waachiliwe.
Rais Magufuli amesema hayo leo Alhamisi Julai 18, 2019 wakati akizungumza na wananchi wilayani Kongwa mkoani Dodoma
Amesema baada ya kutoa maagizo kwa wizara ya sheria, alipokuwa mkoani Mwanza kwa ziara ya kikazi, maofisa wa wizara hiyo walikwenda katika gereza la Butimba jana Jumatano Julai 17 mwaka 2019 na kukaa na watuhumiwa hao kwa saa saba, ambapo baada ya mazungumzo hayo watuhumiwa mbalimbali waliachiwa.
Aidha Rais Magufuli ameeleza baada ya maofisa wa wizara hiyo kutembelea katika magereza mbalimbali, jumla ya watuhumiwa 300 waliokuwa wanashikiliwa kimakosa wameachiwa huru ambapo katika gereza la Butimba watuhumiwa 75 waliachiwa kutoka mahabusu.
“Wilayani Bariadi wameachiwa watuhumiwa 100, Mugumu Serengeti watuhumiwa 52, Tarime watuhumiwa 6, Bunda watuhumiwa 24 na Kahama watuhumiwa 43 wameachiwa” amesema Rais Magufuli.
Rais Magufuli ameeleza maofisa hao wanaendelea kupitia kila gereza kufanya uhakiki kwa watu wanaoshikiliwa kimakosa waachiwe, na leo Alhamisi maofisa hao watakuwa kwenye gereza la Kasungamile na Geita.
Aidha, Rais Dk. John Magufuli ameonekana kumsifu Mbunge wa jimbo la Kongwa, Job Ndugai baada ya kusema kuwa Mbunge huyo anatosha kuliongoza jimbo hilo na kwamba haina haja ya kumchagua kiongozi mwingine kwani mbunge huyo anaisaidia nchi nzima kwa nafasi yake aliyo nayo.
Ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 18, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Jimbo la Kongwa mkoani Dodoma, ambapo amewataka wagombea waliogombea nafasi ya ubunge 2015, kuachana na mawazo ya kutaka kugombea tena kwani nafasi hiyo ni ya Ndugai.
“Ninawashukuru kwa kumchagua Mbunge wenu Ndugai, maana wakati mwingine ni vigumu kwa mtu wa pale pale watu wakajua huyu ni mfalme ndiyo maana katika maandiko wafalme wengi walikataliwa maeneo walipozaliwa lakini ninawambia kuwa mmechagua mtu ambaye anasaidia nchi nzima kwa nafasi yake na msingemchagua kuwa mbunge kwa vyovyote asingekuwa spika,” amesema.
“Ninafahamu wakati wa kampeni kulikuwa na wengine waliohitaji ubunge na nilipofika hapa niliwaambia kazi si ubunge na ukweli ni kwamba wale wote waliogombea niliwateua nafasi mbalimbali wengine wakawa wakurugenzi na wengine wakuu wa mikoa hivyo nitashangaa sana kama 2020 watakuja tena kugombea hapa na wakija wajue hizo nafasi zilizowapa hawataziona tena labda wajitokeze wengine,” amesema.
Aidha, Rais Magufuli amesema kuwa muda umefika wa kulienzi Jimbo la Kongwa kutokana kubeba historia ya Tanzania katika ukombozi wa nchi za kusini mwa Afrika
“Unapotamka Kongwa kwenye nchi ambazo zimepata uhuru kutokana na kujitolea kwenu wanaelewa, wapo walioacha hata damu zao hapa na wengine walizikwa hapa, baba wa taifa alipoamua kuzikomboa nchi zote za kusini mwa Afrika alitumia Kongwa kwa hiyo hapa kuna historia ya ukombozi.
“Ninakubaliana na ombi la spika kuwa wakati umefika wa kuienzi Kongwa hata kama ni kwa kuwa na jengo ambalo litakumbusha haya au uwanja wa ndege alioutumia Rais wa Misri na Algeria na nitakapokutana na marais hawa nitawaeleza kwamba kuna uwanja waliutumia viongozi wenu lakini bado haupo vizuri, nitachomekea chomekea,” amesema Rais Magufuli.
Aidha, Rais Magufuli aliendesha zoezi fupi la uchangishaji kwa shule ya msingi Sagara iliyoepata uharibifu kutokana na dhoruba ya kimbunga. Viongozi mbalimbali walishiriki waliokuwepo katika ziara hiyo kuchangia ambapo Mhe. Rais Magufuli alitoa kiasi cha shilingi milioni 5 na kuagiza uongozi wa Halmashauri usimamie kikamilifu fedha zilizokusanywa.
Aidha, Rais Magufuli ameagiza kuharakisha kwa zoezi la utangazaji zabuni ya ujenzi wa barabara ya maungio ya Kongwa kwenda Mpwapwa ili kujibu kilio cha wananchi wa Mpwapwa cha kupata barabara ya kiwango cha lami, ambapo amemuagiza Meneja wa TANROAD Mkoa wa Dodoma kukamilisha zoezi hilo ndani ya mwezi huu wa saba.
Aidha, Rais Magufuli amejibu kilio cha wananchi wa eneo la Mbande Wilayani Kongwa kwa kuagiza eneo la TARIRI (PRC) limegwe na kutumika kwa ujenzi wa kituo cha mabasi pamoja na kituo cha polisi. Mhe Rais amesema ameagiza hayo wakati akielekea Jijini Dodoma aliposimama Mbande kuongea na wananchi. Aidha, Mhe Rais Magufuli ametoa kiasi cha fedha shilingi milio 5 tasilimu kilichopokelewa na Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Dodoma ambazo zitatumika kuanzisha ujenzi wa kituo cha polisi Mbande na wananchi walimuhaidi Mhe Rais kuwa watachangia ujenzi huo.
Aidha, Mhe Rais Magufuli ameagiza Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Jinsia, Wazee na Watoto kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni 100 kuanzisha ujenzi wa Kituo cha Afya Mbande.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.