Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa kupitia Divisheni ya Maendeleo ya Jamii imefanya uzinduzi wa ugawaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo.
Katika kipindi cha takriban miezi nane Halmashauri imefanikiwa kusajili jumla ya Wafanyabiashara ndogondogo 618 katika mfumo wa WBN ikiwa inajumuisha wanawake 279 na wanaume 349. Usajili huu umetekelezwa na Divisheni ya Maendeleo ya Jamii kwa kushirikiana na Kitengo cha Biashara na Kitengo cha Tehama Wilaya ya Kongwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa imepokea jumla ya vitambulisho 117 kati ya 297 vilivyolipiwa ikiwa ni awamu ya kwanza ya utoaji wa vitambulisho hivi ambavyo utoaji wake ni endelevu kwa kadri malipo yatakavyopokelewa na Wizara iliyopewa dhamana ya uzalishaji wa vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo.
Akiongea na wafanyabiashara waliojitokeza kupokea vitambulisho vyao, Mkuu wa Divisheni ya Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Kongwa Bi. Pascalina Duwe amebainisha faida anazopata mfanyabiashara ndogondogo pindi anapokuwa na kitambulisho, ikiwa ni Pamoja na kutambulika na mamlaka mbalimbali ikiwa ni Pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri husika na taasisi za kifedha.
Pia faida nyinginezo ni Pamoja na kutambuliwa na kupata mikopo katika taasisi mbalimbali za kifdha hapa nchini ikiwemo NMB bank ambayo imepewa dhamana ya kutoa mikopo yenye thamani ya Bilioni 18.5 kwa wafanyabiashara ndogondogo.
Aidha zoezi la usajili wa wafanyabiashara ndogondogo ni endelevu hivyo wananchi wenye sifa wanasisitizwa kuendelea kujisajili kwa ajili ya kupata vitambulisho ili waweze kunufanika na fursa mbalimbali zitokanazo na vitambulisho vya wafanyabiashara ndogondogo.
Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya
Anuani ya Posta: S.L.P 57 Kongwa, Dodoma
Simu ya Mezani: +255 26 2370031
Simu ya Mkononi: +255 713399349
Barua pepe : ded@kongwadc.go.tz
Copyright ©2022 Kongwa District Council . All rights reserved.